Sababu Kumi Kwa Nini Ni
Muhimu Wewe Kuwa na Blog.
Blog ni sehemu ndogo ya
mtandao wa internet ambapo
unaweza kuweka maoni au
maandiko yako na yakaonekana
dunia nzima. Tofauti na website
(tovuti), blog ni rahisi kuanzisha,
rahisi kuendesha na haihitaji
gharama kubwa, unaweza
kuendesha bure kabisa.
Kuna faida nyingi sana za wewe
kuwa na blog, katika makala,
tengeneza blog yako leo na upate
faida hizi tano niliongelea faida za
kiuchumi za kuwa na blog. Leo
nitaongelea faida za maendeleo
yako binafsi kwa kuwa na blog
yako. Hapa nazungumzia blog za
kuandika mambo yenye msaada
kwa watu wengine na sio za
kuripoti habari za udaku.
Hizi hapa ni sababu kumi kwa
nini ni muhimu wewe kuanzisha
blog yako leo hii na sasa hivi;
1. Kuendesha blog ni changamoto
na changamoto zinakufanya
ukue.
Wote tunajua kwamba bila ya
changamoto huwezi kukua kiakili
na kimawazo. Unapokuwa na blog
na kujiwekea ratiba ya kuandika
kwenye blog yako kuna wakati
inakuwa vigumu kabisa kwako
kuweza kuandika kitu chenye
maana. Lakini kama utaweza
kukaa chini na kuandika hata
kama hujisikii kuandika
inakujengea nidhamu kubwa na
utaweza kufanya mambo mengine
makubwa kwenye maisha yako.
2. Kujifunza mambo mapya.
Kuwa na blog ni sehemu nzuri
sana ya kujifunza mambo mazuri
tena kwa bure kabisa. Kwanza
kabisa utajifunza kuandika kitu
ambacho kitakusaidia sana
kwenye shughuli zako. Pili
utajifunza zaidi kuhusu mada
unazopendelea kuandika. Kwa
njia hii utajua mengi zaidi na
yatakusaidia kwenye kazi na
biashara zako.
3. Kuleta tofauti kwenye maisha
ya watu.
Chochote utakachoandika kwenye
blog yako ambacho kinakusaidia
wewe, jua kuna mtu mwingine pia
akikisoma kitamsaidia sana. Kwa
kuandika mambo ambayo
yanawasaidia watu na
wakakutafuta kukushukuru kwa
maandiko yako inakupa moyo na
kukufanya uandike zaidi. Hii
imekuwa ikitokea kwangu karibu
kila siku.
4. Unakuwa mtaalamu.
Unapokuwa na blog na ukachagua
mada fulani ukawa unaziandikia
mara kwa mara itakufanya wewe
kuwa mtaalamu wa mada hizo, na
baadae watu watakufuata kwa
ushauri. Kwa mfano kama una
blog na unaandika kuhusu kilimo
na ufugaji watu watakapokuona
ukiandika kwa muda mrefu
inakuwa rahisi kwao kukufata na
kutaka ushauri zaidi kuhusiana na
mambo hayo. Kwa njia hii
unaweza kutengeneza biashara
nzuri baadae.
5. Unayaweka mawazo yako
kwenye mtandao mkubwa.
Kwa kuwa na blog
iliyounganishwa na mitandao ya
kijamii ni rahisi kwa watu
kusambaza ujumbe wako kwenye
mitandao yao. Kama unaandika
vitu vyenye msaada kwenye
maisha ya watu ni rahisi kwao
kuwashirikisha wengine. Hii
itakuza sana blog yako na
itatengeneza fursa ya biashara
baadae.
6. Kujenga uzoefu mpya.
Kama umeajiriwa na kazi yako
haina hamasa kubwa ni rahisi
sana kuwa na msongo wa
mawazo. Ila kama ukiwa na blog
yako unakuwa na uzoefu mpya
ambapo utakuwa na utaratibu wa
kujifunza zaidi, kuandika na
kushirikisha dunia mawazo yako.
Pia itakuwa rahisi kwako
kujadiliana na wasomaji wako
kuhusu mada mbalimbali. Hivyo
badala ya kutumia internet yako
au ya ofisi kwa kuangalia mambo
yasiyo na maana kwenye
mtandao, hebu anzisha blog yako
leo na uanze kufurahia maisha
yako.
7. Kukutana na watu wapya.
Kwa kuwa na blog inayoandika
mambo mazuri inakuwa rahisi
sana kwako kukutana na watu
wapya na wa muhimu sana
kwenye mada unazoandika na
hata biashara. Kupitia blog
nimeweza kukutana na watu
wengi sana ambao mpaka sasa
tunashirikiana kibiashara na
katika mambo mengine muhimu
ya maendeleo.
8. Kuandika kuhusu maisha yako.
Kuwa na blog sio lazima uandike
mada kwa ajili ya watu wengine.
Unaweza kuwa na blog
utakayoandika safari ya maisha
yako. Uzuri ni kwamba unaweza
kuifanya blog kuwa private hivyo
ukaiona wewe tu au watu
utakaowaruhusu waione.
9. Kukabiliana na hofu zako.
Blog ni njia moja nzuri sana ya
kukabiliana na hofu zako. Kama
una hofu ya kupingwa hivyo
unashindwa kutoa maoni yako
kwenye vikao muhimu anzisha
blog yako leo. Mada yoyote
utakayoandika kwenye blog yako
lazima kuna mtu atakupinga, kwa
njia hii utajifunza kukabiliana na
upinzani wa aina hii na moja kwa
moja unaondoa hofu ya kupingwa.
Moja ya makala nilizokuwa
naandika mwanzoni kabisa
wakati naanzisha AMKA
MTANZANIA ni umuhimu wa watu
kujisomea vitabu ili kujiendeleza
binafsi. Nilipata upinzani mkubwa
sana kutoka kwa baadhi ya watu
kama vile niliwashikia fimbo na
kuwalazimisha. Iliniumiza sana
mwanzoni lakini baadae
nilijifunza ni sehemu ya uandishi.
10. Kutengeneza fursa za
kibiashara.
Kuwa na blog ni njia rahisi ya
kutengeneza fursa mpya za
biashara. Unaweza kutafutwa
kutokana na utaalamu wako
kwenye mada unayoandika na
kuwa mshauri mzuri. Unaweza
kuuza bidhaa zako zinazotokana
na mada unayoandika kupitia blog
yako. Kuna fursa nyingi za
kibiashara utazipata kwa kuwa na
blog.
Kama mpaka sasa huna blog
anzisha blog yako leo. Sahau
chochote kuhusu biashara au
kutengeneza fedha kupitia blog
hiyo. Anza kwa kutengeneza
utaalamu wako kupitia mada
unayochagua kuandika, baadae
fedha zitakufuata zenyewe.
Huna utaalamu wa kuanzisha
blog? Usihofu, kila kitu kiko hapa.
Kama umeweza kusoma hapa
basi nakuhakikishia unao uwezo
wa kuanzisha blog yako chini ya
nusu saa. Unachohitaji ni kuwa
na kompyuta na internet, baada
ya hapo utafuata maelekezo
rahisi na yenye picha kwenye
KISIMA CHA MAARIFA na
kukamilisha blog yako ndani ya
muda mfupi. Kama bado
hujajiunga na kisima cha maarifa
bonyeza maandishi hayo ya jina
na utapata maelekezo ya kujiunga
na kisima. Kwa shilingi elfu kumi
tu za kitanzania utaweza kupata
maarifa muhimu ambayo
yatakusaidia sana kuboresha
maisha yako. Utajifunza jinsi ya
kutengeneza na kukuza blog,
kuwa mwandishi mzuri,
kuanzisha na kukuza biashara na
mengine mengi muhimu. Karibu
sana.
Good
ReplyDelete